Ruto: Wakenya zaidi ya milioni 31 wamejisajili na SHA

Martin Mwanje
1 Min Read

Jumla ya Wakenya milioni 31.5 wamejisajili na Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA. 

Rais William Ruto amesema kati ya waliojisajili, 800,000 ni wakazi wa kaunti za Wajir, Garissa na Mandera.

Amesifia idadi kubwa ya Wakenya wanaojisajili na mpango huo akiitaja kuwa upanuzi mkubwa wa huduma za matibabu nchini kote tangu taifa hili lilipojinyakulia uhuru.

“Hadi leo, SHA imelipa shilingi bilioni 8.1 kwa hospitali zinazowahudumia Wakenya katika kaunti hizi tatu, ikiashiria athari ya mageuzi haya kwa upatikanaji wa huduma bora za afya,” alisema Rais Ruto wakati akiliongoza taifa kuadhimisha Sikukuu ya Madaraka katika kaunti ya Wajir.

Aliyasema hayo wakati ambapo hutoaji huduma za matibabu chini ya SHA umeibua hisia mseto miongoni mwa Wakenya.

Ingawa kuna wale wanaosema mpango huo umesaidia kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, kunao wanaodai umefanya iwe vigumu kwa wengi kupata huduma hizo.

Baadhi ya hospitali pia zimeripotiwa zikidai malipo kwa huduma zilizotolewa kitambo kile.

Serikali inasema imeweka mfumo madhubuti kuhakikisha hakuna ulaghai unatokea chini ya SHA.

 

Share This Article