Vijana wajasiriamali 88,934 kote nchini wanapokea shilingi zilizosalia 25,ooo chini ya mradi wa NYOTA ili kuwawezesha kuboresha biashara zao mbalimbali walizoanzisha.
Hii inafanya jumla ya fedha walizopokea kufikia sasa kuwa shilingi 50,00o kwani walipokea shilingi 25,000 katika awamu ya kwanza ya mpango huo.
Vijana wengine 33,269 wanapokea shilingi 25,000 kwa mara ya kwanza wanapotia guu katika safari yao ya ujasiriamali.
“Kwa pamoja, vijana wajasiriamali zaidi ya 122,000 katika kaunti zote 47 hii leo wanapokea msaada wa biashara wa zaidi ya shilingi bilioni 3.05,” alisema Rais Ruto wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika uwanja wa Ulinzi jijini Nairobi leo Ijumaa.
“Huu ni mmoja wa uwekezaji mkubwa zaidi ulioratibiwa kuwahi kufanywa katika vijana wajasiriamali nchini Kenya kwa sababu tunaamini kwamba kuwekeza katika biashara ni kuwekeza katika mustakabali wa uchumi wetu.”

Akizindua awamu ya pili ya mradi huo, Rais Ruto aliagiza Wizara ya Vyama vya Ushirika kuanzisha mbinu ya kitaifa ya utambuzi wa NYOTA ili kila anayenufaika aweze kupata huduma za serikali, ruzuku na fursa zinazokusudia kuunga mkono ukuaji wa biashara.
Pia aliagiza taasisi za kifedha za serikali ikiwa ni pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Mfuko wa Uwezo na ule wa Wanawake na mashirika mengine ya serikali kuanzidha Bidhaa ya Ukuaji mahususi wa NYOTA.
Alirejelea biashara mbalimbali zilizoanzishwa na vijana nchini kote tangu kuzinduliwa kwa awamu ya kwanza ya mradi wa NYOTA akisema hiyo ni ishara tosha kwamba mradi huo umefanikiwa.
Mradi wa NYOTA ni mpango wa serikali unaonuia kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapa mtaji wa kuanzishia biashara.
Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia.