Magwiji wa muziki wa Kenya, Jua Cali na Nyota Ndogo, ni miongoni mwa wasanii wa kimataifa wanaotarajiwa kutumbuiza katika maadhimisho ya miaka 30 ya muziki wa Bongo Flava, almaarufu ‘Bongo Flava @30’.
Hafla hiyo ya kihistoria inaandaliwa usiku wa leo Julai 10, 2026, katika eneo la Mlimani City jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Tamasha hilo la kihistoria linakutanisha waanzilishi wa Bongo Flava kusherehekea safari ya muziki huo tangu ulipoanza miaka ya 1990 hadi kuwa moja ya bidhaa kubwa zaidi za muziki barani Afrika.
Ushiriki wa wasanii hao wawili kutoka Kenya unaonyesha uhusiano wa muda mrefu wa kimuziki kati ya Kenya na Tanzania.
Nyota Ndogo aliwasili Dar es Salaam mapema wiki hii na kusema mwaliko wake ni ishara ya uhusiano wa kihistoria uliowahi kuwaunganisha wasanii wa nchi hizo mbili.
Naye Jua Cali, anayefahamika kama mwanzilishi wa muziki wa Genge nchini Kenya, aliwasili Dar es Salaam jana, baada ya kuthibitisha ushiriki wake awali kupitia ujumbe wa video.
Waandalizi wanasema maadhimisho hayo si tu ya kusherehekea urithi wa Bongo Flava, bali pia ni jukwaa la kukutanisha tena wasanii walioweka msingi wa mafanikio ya muziki huo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Paul Makonda, alihimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi awali, na kulingana na Babu Tale, tiketi zote tayari zimeuzwa.