Bimbo Ademoye alalamikia matumizi ya kazi zake bila idhini nchini Ghana

Hii ni baada ya vituo vya runinga nchini Ghana kupeperusha filamu zake alizochapisha kwenye mtandao wa YouTube bila idhini.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji wa filamu nchini Nigeria Bimbo Ademoye ambaye pia ni mwandalizi wa filamu amelalamikia kile anachokitaja kuwa matumizi ya kazi zake bila idhini na vyombo vya habari nchini Ghana.

Katika malalamiko aliyochapisha kwenye akaunti yake ya Instagram na kuhusisha maafisa kadhaa wa Ghana Ademoye alilalamikia hatua ya vituo vya runinga vya Ghana ya kuonyesha filamu zake alizochapisha kwenye YouTube bila idhini yake.

Baadaye, Bimbo alichapisha video ya raia mmoja wa Ghana anayemkashifu kwa kulalamika akidai kwamba vituo hivyo vya runinga vya Ghana vinamsaidia kutangaza kazi zake.

“Kwanza ningeenda kuomba msamaha kwa mashabiki wangu na familia hasa babangu” aliandika Bimbo akiendelea kusema kwamba babake angependelea aache kuzungumzia suala hilo lakini wakati mwingine, “lazima adondoshe taji yake na aingilie uchafu”.

Alielezea jinsi alikuwa amelalamikia uchapishaji wa filamu zake uliotekelezwa na vituo vya runinga vya Ghana bila idhini lakini wengine wameamua kumdhalilisha wakidai kwamba vituo hivyo vinamsaidia.

Waziri wa mawasiliano, uchumi dijitali na ubunifu nchini Ghana Sam Nartey George na afisa mkuu mtendaji wa mamlaka ya filamu nchini Ghana Kafui danku hata hivyo wamemhakikishia Bimbo kwamba hatua mwafaka zitachukuliwa.

Danku aliandika chini ya chaisho la Ademoye ambapo alisema, “Kwa ushirikiano na usimamizi wangu ninashughulika ili kukomesha hatua hii na utaona mabadiliko katika muda wa wiki chache zijazo.”

Waziri Sam Nartey George naye alisema atachunguza suala hilo akisisitiza kujitolea kwa serikali kuhakikisha utunzaji wa hakimiliki.

Website |  + posts
Share This Article