Mwanamuziki mkongwe nchini Uganda Bebe Cool amezungumzia malalamishi yanayoongezeka ya wasanii wanaodai kutopokea malipo licha ya kutumbuiza kwenye mikutano ya kampeni ya Rais Yoweri Kaguta Museveni.
Hatua hii inafuatia lalama za hadharani za wasanii kama Gravity Omutujju na Buchaman kwenye vyombo vya habari na hata mitandao ya kijamii.
Akizungumza mubashara kwenye TikTok Bebe Cool, ambaye alikuwa akisimamia wasanii katika kampeni ya Rais Museveni, alikiri kucheleweshwa kwa malipo ya baadhi ya wasanii akisema malipo hayajafanywa hadi sasa.
Cool alisema kwamba anatarajia kupata mwafaka kuhusu suala hilo hivi karibuni baada ya kushauriana na mamlaka husika, labda akimaanisha usimamizi wa chama tawala cha NRM.
Bebe Cool sasa anaomba wasanii husika wasalie kuwa na subira, akisisitiza kwamba jinsi watashughulikia masuala kama hayo, huenda ikaathiri fursa zijazo.
“Iwapo mtu atakupa fursa ya kufanya kazi, ni muhimu kudhihirisha subira na tabia njema,” alisema Bebe Cool akifafanua kwamba iwapo watafanya hivyo, mtu huyo atakapokuwa na fursa nyingine hatakuwa na shida kulipa baadaye.
Alipongeza wasanii na wanahabari kwa kusalia imara hata wakati wa misukosuko kama hii akielezea kwamba mchakato mzima wa kupata kazi kama hizo huwa mgumu.
Hivi maajuzi mwanamuziki Gravity Omutujju alitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Bebe Cool kwa kukosa kulipwa akisisitiza kwamba aliingia kwenye mkataba naye.