Chama cha United Democratic Alliance, UDA kimefanikiwa kuendesha uchaguzi wake wa mashinani katika Kaunti ya Wajir, huku maafisa wakiripoti kwamba zoezi zoezi hilo halikuwa na matatizo.
Akizungumza baada ya kufungwa kwa shughuli ya kupiga kura, afisa wa UDA Salma Ochieng alisema uchaguzi huo, uliofanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni, ulidhihirisha mwitikio mkubwa katika vituo vyote vya kupigia kura kaunti nzima.
Ochieng, ambaye alikuwa ameandamana na Afisa Mkuu wa uchaguzi katika Kaunti Gladys Chebet na afisa wa chama Victor Mtai, alibainisha kuwa zoezi hilo lilifuatia kampeni ya uhamasishaji ya wiki moja iliyolenga wanachama wa chama na wanaowania nyadhifa.
“Tangu Jumatatu tumekuwa hapa tukihamasisha kuhusu uchaguzi wa mashinani wa UDA katika ngazi ya vituo vya kupigia kura. Leo tumefanikisha uchaguzi huo na sasa tumefunga vituo vyote vya kupigia kura katika Kaunti ya Wajir,” alisema Ochieng.
Aliongeza kuwa chama hicho kinajizatiti kuanzisha miundo ya uongozi katika ngazi ya mashinani kulingana na matakwa ya kisheria, akibainisha kuwa uchaguzi huo ulilenga makundi saba ya wawakilishi katika ngazi ya vituo vya kupigia kura.
“Haya ni pamoja na makundi ya maslahi maalum, wawakilishi wa wanachama, wawakilishi wa wakulima, wa dini, wataalamu, biashara ndogo na za kadri na wawakilishi wa vijana,” alieleza.
Afisa huyo alieleza pia kuridhishwa na namna zoezi hilo liliendeshwa, akisema kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na haukugubikwa na changamoto zozote kubwa.
“Tunafurahia kwamba uchaguzi umefanyika kwa amani kote kaunti nzima. Hatukupata matatizo yoyote, na tunawashukuru wanachama wote waliojitokeza kushiriki,” alisema.
Ochieng aliwapongeza wote waliojitokeza kuwania nyadhifa na wapiga kura kwa kushiriki katika zoezi hilo, akilitaja mchakato huo kuwa mafanikio kwa juhudi za chama kuimarisha mizizi yake mashinani.