Wanagenzi zaidi ya 6,784 katika sekta ya afya wamekabidhiwa barua za kuhudumu katika vituo mbalimbali vya aftya kote nchini.
Wataanza kuhudumu Julai 1 mwaka huu chini ya kundi la uanagenzi la mwaka 2026/2027.
Hafla ya kuwakabidhi barua hizo iliongozwa na Waziri wa Afya Aden Duale na kuhudhuriwa na maafisa wa Chama cha Madaktari nchini, KMPDU leo Jumatatu.
Akiwakabidhi barua hizo, Duale alitaja hatua hiyo kuwa muhimu katika azima ya serikali ya kuimarisha nguvukazi katika sekta ya afya na upatikanaji wa afya kwa wote (UHC) chini ya mpango wa serikali wa kutoka chini hadi juu (BETA).
Wanagenzi hao watakaotumwa kuhudumu katika kaunti zote 47 wanajumuisha maafisa wa utabibu 875, madaktari wa meno 69, wafamasia 616 na wauguzi 2,424 miongoni mwa wengine.
Waziri Duale amedokeza kuwa serikali imetenga shilingi bilioni 9.316 kuunga mkono mpango huo katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Duale pia alisisitiza dhamira ya serikali kuimarisha nguvukazi katika sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na kuwaajiri wafanyakazi wa UHC kwa masharti ya kudumu.