Rais William Ruto leo Jumatatu amezindua rasmi barabara ya juu ya Ngong-Naivasha iliyojengwa kwa kitita cha shilingi bilioni 3.58 katika eneo la Junction Mall jijini Nairobi.
Kwenye uzinduzi huo, kiongozi wa taifa alisema barabara hiyo itatatua changamoto ya msongamano wa magari, ambayo imedumaza ukuaji wa jiji la Nairobi kwa miongo kadhaa.
“Lengo letu ni kujenga miundombinu ambayo inabuni jiji la kisasa na lenye ushindani duniani, na kulifanya kiingilio cha Afrika Mashariki,” alisema Rais Ruto.

Mradi huo, uliojengwa na halmashauri ya barabara za miji nchini Kenya -KURA na kufadhiliwa kupitia mkopo kutoka kwa shirika moja la kimataifa la Uhispania, umeundwa ili kupunguza msongamano wa magari kwenye makutano ya barabara ya Ngong-Naivasha.
Rais Ruto aliwakosoa wanasiasa wanaotumia miradi ya maendeleo kushutumu serikali akisema utawala wake unatimiza ahadi zake kwa Wakenya.
KURA inasema barabara hiyo ya juu, itapunguza muda wa usafiri huku ikitoa nafasi kwa waendesha baiskeli na watembea kwa miguu.