Shabiki sugu wa timu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC Michel Nkuka Mboladinga, almaarufu Lumumba Vea, ukipenda Patrice Lumumba, aliwasili kwenye fainali za Kombe la Dunia na kuhudhuria mchuano kati ya DRC na Colombia mapema Jumatano katika uwanja wa Guadalajara, Mexico.
Mboladinga aliyepata umaarufu kwa kusimama dakika zote 90 za mechi wakati wa fainali za kombe la mataifa ya Afrika, AFCON mwaka jana alikosa mchuano wa ufunguzi wa DRC kutokana na sheria za kuwaweka karantini mashabiki wote wanaowasili kutokea DRC kwa Kombe la Dunia.
Shabiki huyo aliye na umri wa miaka 49, hata hivyo hataonyeshwa kwenye runinga wakati wa Kombe la Dunia kutokana na sheria kali za FIFA, zilizopiga marufuku matangazo ya kisiasa uwanjani.

Mboladinga husimama juu ya stuli akiwa ameinua mkono dakika zote 45 za kila kipindi cha mechi za timu ya taifa ya DRC ukipenda The Leopards.
Shabiki hiyo huinua mkono kama ishara ya kuunga mkono Waziri Mkuu wa kwanza wa DRC Patrice Lumumba aliyeuawa kwa sababu za kisiasa.
Hata hivyo, Mboladinga leo ameibuka na mtindo mpya akiinua mkono na kuashiria ishara ya kujipiga risasi kukemea hatua ya kupigwa risasa kwa marehemu Lumumba.