Miili yagunduliwa karibu na kambi ya jeshi ya Mali baada ya raia wengi kukamatwa

Marion Bosire
3 Min Read

Miili iligunduliwa karibu na kambi ya kijeshi ya Mali siku chache baada ya jeshi la nchi hiyo na mamluki wa Urusi kukamata raia kadhaa, kulingana na walioshuhudia waliohojiwa na shirika la habari la AFP.

Mali, inayotawaliwa na serikali ya kijeshi kufuatia mapinduzi ya mwaka 2020 na 2021, imekuwa ikikabiliwa na ukosefu mkubwa wa usalama kwa zaidi ya muongo mmoja, hali inayochochewa zaidi na wapiganaji wa Kiislamu wanaohusishwa na Al-Qaeda na kundi la Islamic State.

Viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo wamevunja ushirikiano wa muda mrefu na mtawala wa kikoloni, Ufaransa na sasa wameelekeza ushirikiano wao kwa Urusi.

Serikali hiyo ya kijeshi hutumia huduma za kile wanachodai kuwa wakufunzi wa kijeshi kutoka Urusi, lakini kwa mujibu wa wataalamu na waangalizi mbalimbali, hao ni mamluki kutoka kampuni binafsi ya Urusi iitwayo Wagner.

Mnamo Aprili 12, wanajeshi wa Mali na mamluki wa Urusi walikamata wanaume kadhaa sokoni katika eneo la Sebabougou, kusini magharibi mwa nchi hiyo na kuwasafirisha hadi kambi ya kijeshi ya Kawla kwa mujibu wa manusura wawili waliokimbilia Mauritania.

Shahidi wa kwanza alisimulia kwamba yeye na wanaume wengine walihojiwa kuhusu uhusiano wao na makundi ya jihad na kuongeza kuwa walichapa watu viboko.

Alieleza kuwa mamluki wa Urusi walimtoa yeye na wengine kambini ili wauwawe.

“Wanajeshi wazungu walitupiga risasi kwa mafundo. Nilianguka kama wengine. Wanajeshi hao waliondoka haraka sana. Sikuwa nimekufa, lakini nililala pale kwa saa kadhaa. Niliona karibu miili 70.” alisema shahidi huyo.

Shahidi wa pili, ambaye pia alikimbilia nje ya nchi alisema alinusurika kuuawa. “Nilikuwa kwenye kundi lililobaki kambini wakati wengine walipelekwa kuuawa.”

Shahidi wa tatu alisema alikwenda karibu na kambi hiyo Jumatatu kutafuta jamaa zake waliokamatwa, “Tulichokiona kilikuwa cha kutisha. Miili, watu waliouawa, raia” Alisema.

Kama mashuhuda wengine na wakazi wa Sebabougou, naye alikimbilia Mauritania.

Shirika moja la kijamii la eneo hilo liliiambia AFP Jumatano kuwa lina orodha ya watu 65 ambao wamepotea hadi sasa, wengi wao wakiwa wa kabila la Fulani.

Shirika hilo ambalo halikutaka kutambuliwa liliongeza kuwa mashuhuda waligundua miili iliyokuwa imetawanyika kila mahali, ikiwa inaoza.

Watu wa kabila la Fulani ni wafugaji wa kuhamahama na mara nyingi wamekuwa wakidharauliwa katika eneo la Sahel, wakituhumiwa kwa kushirikiana na makundi ya Kiislamu yenye misimamo mikali.

Jeshi la Mali limeongeza operesheni zake katikati mwa nchi hiyo katika miezi ya hivi karibuni, likishirikiana na Wagner.

Pia wanatuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia, hasa kutoka jamii ya Fulani.

Mnamo Februari, takriban raia 20 waliuawa katika eneo la Kaskazini mwa Mali magari yao yalipolengwa na wanajeshi na mamluki kulingana na taarifa.

Website |  + posts
Share This Article