Prezzo awasili Tanzania kwa 30 ya Bongo Fleva

Yeye ni miongoni mwa Wageni waalikwa watakaoshiriki maadhimisho hayo.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Kenya Jackson Ngechu Makini maarufu kama Prezzo, yuko katika mkoa wa Mwanza nchini Tanzania kwa ajili ya tamasha ya maadhimisho ya Miaka 30 ya muziki wa Bongo Fleva.

Hafla hiyo itafanyika kesho, Agosti 8, 2026 katika ukumbi wa The Climax, ndani ya jumba la Rock City.

Tamasha hiyo inatarajiwa kuwakutanisha wasanii mbalimbali wa Bongo Fleva katika usiku maalum wa kusherehekea miaka 30 ya muziki huo na mchango wake katika kukuza tasnia ya burudani Nchini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kuwasili, Prezzo amesema amefurahishwa na umoja ulioonyeshwa na Wasanii wa Tanzania katika kuandaa na kushiriki tamasha hiyo, akieleza kuwa hatua hiyo ni mfano wa kuigwa.

Amesema mafanikio ya tamasha hiyo yamewapa hamasa Wadau wa muziki Nchini Kenya kuanza maandalizi ya kuanzisha tamasha ya aina hiyo itakayowaunganisha Wasanii wa Kenya, kwa lengo la kuimarisha mshikamano, kubadilishana uzoefu na kuendeleza tasnia ya muziki Nchini humo.

Prezzo ni miongoni mwa Wageni waalikwa watakaoshiriki maadhimisho hayo.

Mwanza ndio mji wa kwanza ambapo tamasha ya miaka 30 ya Bongo Fleva inaandaliwa baada ya tamasha kuu iliyofanyika jijini Dar es Salaam, waandalizi wakipanga kuzuru mikoa mingine nchini humo.

Nyota Ndogo na Jua Cali waliwakilisha Kenya katika hafla kuu ya kuadhimisha miaka 30 ya Bongo Fleva.

Share This Article