Mwanamuziki wa Nigeria Portable amesema anataka pigano la ndondi na Cubana Chiefpriest la Naira milioni 100.
Portable ambaye jina lake halisi ni Habeeb Okikiola alichapisha video ambayo inamwonyesha akisema kwamba yeye anatafuta pesa ndiposa ameamua kupigana mchezo wa ndondi na watu wakubwa wenye hela.
“Hamjambo mabibi na mabwana, ni pesa ninatafuta, nataka kupigana kwa ajili ya pesa. Chiefpriest ndiye nataka kupigana naye” alisema Portable huku akiongeza kwamba Cubana anajua biashara.
Msanii huyo mwenye utata aliendelea kwa kumuuliza Chiefpriest iwapo alijifunza kupiga ndondi akielezea kwamba hana ugomvi naye bali ni pesa tu anatafuta akitaja Naira milioni 100.
Haya yanajiri wiki chache baada ya Portable kutangaza kwamba anataka kupambana na bingwa wa zamani wa ndondi wa uzani wa juu mara mbili, Anthony Joshua.
Alikuwa anajigamba baada ya kushinda kwenye pambano la ndondi la nyota wa muziki dhidi ya Darlington Okoye maarufu kama Speed Darlington.
Wakati wa shindano hilo kati ya Portable na Speed Darlington, Portable alimrushia Darlington makonde ya haraka-haraka, akionyesha hatua za miguu za wepesi na mashambulizi yasiyokwisha.
Pambano hilo lilimalizika ghafla baada ya Speed Darlington, aliyekuwa na bandeji kwenye mkono wa kulia, kukataa kuendelea na raundi ya pili, hivyo kumpa Portable ushindi kwa Technical Knockout.
Baada ya pambano, Speed Darlington alimtuhumu Portable kwa kutumia nguvu za kishirikina wakati wa pambano hilo.
Wakili wake kwa jina Deji Adeyanju, alitaka pambano lirudiwe, akidai uamuzi mbaya kutoka kwa waamuzi na kutaka raundi ya pili yenye haki.