Mwanamuziki wa Kenya Juanita Tunu ambaye anafahamika kwa nyimbo tamu za mtindo wa Afro Pop amezindua video ya wimbo wake unaopendwa wa “Body Tea”.
Mrembo huyo ambaye yuko chini ya usimamizi wa kampuni ya muziki ya Universal Music Group East Africa anaendelea kujikita katika muziki wa Afrika Mashariki.
Wimbo huo wa Body Tea ndio kazi ya kwanza amefanya chini ya kampuni hiyo iliyomsajili hivi maajuzi kufuatia talanta aliyodhihirisha akiwa chini ya mpango wa mafunzo wa Sauti Sol.
Taswira ya video ya wimbo wa Body Tea ni sherehe ya kisinema ya kujiamini na kuwa mwanamke wa kisasa wa Kiafrika. Dada huyo anaonyesha mitindo ya kisasa ya mavazi kwenye video hii ambayo inanasa hisia laini na ya kuvutia.
Densi zake kwenye kazi hiyo ni zenye mvuto na mitindo ya mavazi ikiangazia mageuzi ya Juanita kutoka kipaji chipukizi hadi kuwa nguvu kubwa ya kikanda.
Hajahusisha watu wengine kama wacheza densi au waigizaji kwenye kazi hiyo na hajatumia maeneo mengi na mavazi mengi katika kuiandaa.
Juanita anasema Body Tea inahusu kujiamini na kukumbatia mtindo wako mwenyewe akiongeza kusema, “Kufanya kazi na timu ya UMG EA kwenye taswira hii kuliniwezesha kuleta uhalisia wa hisia na nishati ya wimbo kwa namna inayohisi kuwa halisi kulingana na hatua niliyopo kama msanii kwa sasa.”
Body Tea sasa inapatikana kwa kusikilizwa kwenye majukwaa yote makubwa, na video rasmi ya muziki inaweza kutazamwa kwenye chaneli ya YouTube ya Juanita Tunu.