Mwanamuziki wa Tanzania Harmonize ameshangaza wengi baada yake kukiri kwamba amewahi kuwa na madeni lakini hilo kamwe halikumkwaza maishani ila aliendelea kupambana.
“Kama mlivyosikia nadaiwa baba mwenye nyumba kanijia juu imenibidi nifungashe uzuri nimepata nyumba kali tuu maeneo ya GOBA huku ..!!” aliandika Harmonize.
Aliendelea kusema kwamba yeye hajawahi kuwa mwoga wa madeni huku akiwatia moyo wanaodaiwa madeni akisema, “Usirudi nyuma usijali kilamtu anadaiwa.”
Msanii huyo aliorodhesha madeni aliyowahi kudaiwa ambayo anasema amefanikiwa kulipa katika kipindi cha miaka mitatu, ambayo ni pamoja na milioni 600 za Label(inayoaminika kuwa Wasafi), milioni 200 za benki ya CRDB, Milioni 100 za Dkt. Jembe, milioni 180 za aliyekuwa mke wake Sarah na zaidi ya Bilioni 1 alizowekeza kwenye kampuni yake ya muziki ya Konde.
Baadaye katika chapisho lilo hilo, Harmonize aliorodhesha baadhi ya mali anazomiliki akisema kwamba huwa hapendi kujionyesha mitandaoni.
Alitaja magari kama V8 mbili, Range Rover sport moja, Range Rover defender ya mwaka 2024 moja na BMW 4Z moja pamoja na nyumba ya thamani za zaidi ya shilingi bilioni 4.
Muziki wake pekee alisema una thamani ya dola milioni 5 za kimarekani akishangaa itakuwaje iwapo ataamua kuuza.
Msanii huyo alisema kwa sasa hadaiwi mkopo wowote na wala hataki kukopa na kwamba anaangazia mafunzo au elimu kuhusu fedha na huenda labda akakopa baadaye.