Filamu ambayo mchekeshaji na mwigizaji Crazy Kennar ni mhusika mkuu itazinduliwa hivi karibuni jijini Nairobi.
Filamu hiyo kwa jina “My Name is Omosh” itazinduliwa Februari 15, 2025 saa moja jioni katika ukumbi wa maonyesho ya filamu wa Century Cinemax, katika jumba la kibiashara la Sarit.
Mwelekezi wa filamu hiyo ambaye ni mwanamuziki Kennedy Ombima maarufu kama King Kaka alichapisha bango la ujio wa filamu hiyo na kuandika, “Filamu mpya itakayozinduliwa tarehe 15.”
Kaka aliongeza kusema kwamba alifurahikia jukumu lake la kuelekeza filamu hiyo akiwa na wahudumu wengine kadhaa na waigizaji stadi.
“Asante sana Crazy Kennar na wote waliosaidia kuunda kazi hii. Nasubiri kwa hamu sana mkutane na Omosh.” alimalizia King Kaka.
Kennar naye alichapisha bango lilo hilo akisema “Ninafurahi sana kushiriki nanyi filamu yangu ya kwanza ‘My name is Omosh’. Tuliweka roho zetu kwenye kazi hii. Utaipenda.”
Aliendelea kuelezea kwamba yeye ndiye aliandika mswada wa filamu hiyo, ikaelekezwa na King Kaka na inahusisha waigizaji kama vile Austin Muigai.
Crazy Kennar amekuwa akijihusisha na uundaji na uchapishaji wa video fupi kwenye mitandao ya kijamii na hii ndiyo filamu yake ya kwanza.
King Kaka wa upande wake amewahi kuandaa filamu kama vile Majuto ya mwaka 2020, Kamtupe ya mwaka 2022 na Monkey Business ya mwaka 2024.