Mwanamuziki wa Marekani R. Kelly ameshtakiwa na wahasiriwa wake sita kwa madai ya kukosa kuwalipa fedha alizoagizwa na mahakama.
Kulingana na stakabadhi za kesi hiyo mpya, wahasiriwa hao wanasema kwamba mahakama iliwapa dola milioni 10.3 katika uamuzi dhidi ya mwanamuziki huyo mwaka 2023 na hawajalipwa pesa hizo kikamilifu kufikia sasa.
Lizette Martinez, Lisa Van Allen, Kelly Rogers, Faith Rogers, Roderick Gartrell na Gem Pratts wanadai kwamba kwa jumla pesa ambazo wamelipwa kufikia sasa hata hazifiki dola laki 5.
Waliodhulumiwa na Kelly walijotokeza na kuhadithia kuhusu madhila yao mikononi mwa mwanamuziki huyo kwenye kipindi ‘Surviving R. Kelly’ na sasa wanamwandama yeye na kampuni yake Universal Music wakitaka walipwe fidia.
Uamuzi wa kesi hiyo ulitolewa mwezi Agosti mwaka 2023 lakini akakosa kuridhia akidai kwamba hakufahamu lolote kuhusu kesi hiyo na hafai kuwajibishwa.
Kelly kwa sasa anahudumia kifungo cha miaka 30 gerezani na maswali yamekuwa yakiibuliwa kuhusu iwapo wahasiriwa wake watalipwa fidia waliyozawadiwa na mahakama.
Wakili wa R. Kelly Jennifer Bonjean alielezea wanahabari kwamba uamuzi huo wa mahakama uliafikiwa wakati hakuwa amejiunga na kundi la mawakili la mwanamuziki huyo na rufaa yake bado haijasikilizwa.