Wema Sepetu matatani kisa mavazi!

Ameitwa kwa mahojiano na bodi ya filamu ya Tanzania kutokana na vazi alilovaa katika sehemu ya burudani akiwa na msanii wa muziki Gigy Money.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji wa Tanzania Wema Sepetu amejipata matatani baada ya kuvaa mavazi yanayoaminika kuwa kinyume na maadili na picha zake akiwa amevaa vazi hilo kuchapishwa mitandaoni.

Wema pamoja na mwanamuziki Gigy Money walionekana kwenye picha za pamoja wakiwa wamevaa vazi sawia ila rangi tofauti ambapo Gigy alikuwa amevaa la rangi nyekundu huku Wema akivaa la rangi nyeusi.

Vazi hilo ni la kubana mwili kabisa na linaonyesha ngozi.

Sasa bodi ya filamu nchini Tanzania imemwita Wema kwa kikao Mei 22, 2025 saa nne asubuhi kwa kile ilichokitaja kuwa mahojiano.

Taarifa iliyotiwa saini na kaimu katibu mtendaji wa bodi hiyo Gervas Kasiga inasema, “Bodi imesikitishwa na picha jongevu zisizokuwa na maadili zilizorushwa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha Mwanatasnia Wema Sepetu akiwa katika mavazi yasiyo na staha.”

Iliendelea kusema kwamba bodi hiyo inawasihi wahusika wa tasnia ya filamu nchini Tanzania kuendelea kulinda maadili katika kazi zao na mienendo ya kijamii.

Awali wanamitandao walimrushia maneno Gigy Money wakisema kwamba yeye ndiye alimshawishi Wema kuvaa vazi hilo na hivyo anamharibu.

Money alichapisha picha zao za pamoja na kuandika, “Eti Gigy wa kumuharibu Wema na anamharibu Kama nani?” aliendelea kwa kuwataka wakosoaji wamkome akisema hana uwezo wa kumdhibiti Wema.

Yapata miaka minne iliyopita Gigy Money alijipata matatani kutokana na vazi alilovaa jukwaani wakati wa Wasafi Festival huko Dodoma ambapo alipatiwa adhabu ya kufungiwa kwa miezi sita na Baraza la Sanaa la Taifa.

BASATA hata hivyo haijasema lolote kuhusu tukio la juzi la Wema na Gigy Money.

Website |  + posts
Share This Article