Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi na mwandishi wa Uganda wakili Agatha Atuhaire, wamerejeshwa makwao kutoka nchini Tanzania.
Maafisa wa polisi wamesema wawili hao waliosafiri hadi nchini Tanzania ili kuhudhuria kesi inayomkabili kiongozi wa chama cha CHADEMA nchini humo Tundu Lissu, wamefurushwa Tanzania muda mfupi baada ya kukamatwa.
Mwangi alikamatwa Mei 19, 2025 kwa madai ya kutoa habari za uwongo ili kuruhusiwa kuingia nchini humo.
Kwa mujibu wa polisi wa Tanzania aliwasili nchini humo tarehe Mei 18, 2025.
Mashrika ya wanaharakati yakiwemo yale ya The Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC), kwa ushirikiano wa kituo cha sheria nchini Tanzania (TLS) na shirika kuu la Sheria Afrika Mashariki (EALS), walitoa ushauri wa kisheria kwa wanaharakati hao wawili.
Kutimuliwa kwa wawili hao nchini humo, kunajiri siku chache tu baada ya wanaharakati wengine kutoka Kenya kuzuiwa kuingia nchini Tanzania kuhudhuria kesi dhidi ya Lissu.
Waliozuiwa kuingia Tanzania ni pamoja na aliyekuwa Jaji Mkuu Willie Mutunga, Kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party Martha Karua, na wanaharakati wengine.
Siku ya Jumatatu Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, alionya dhidi ya wanaharakati kuingia nchini mwake na kuvuruga amani.
Kiongozi wa Chama cha CHADEMA Tundu Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini.