Mwanamume mmoja ameripotiwa kufariki katika mahakama ya Bungoma leo Jumanne wakati akimsubiri wakili wake kuwasili ili kupisha kusikilizwa kwa kesi yake.
Idara ya Mahakama inasema mwanamume huyo aliletwa mahakamani akiwa amebebwa kwa baiskeli na kwamba hakuonekana buheri wa afya.
Alikuwa na kesi kwenye mahakama ya mazingira na ardhi na aliashiria kuwa atamsburi wakili wake ili kujua mwelekeo wa kesi hiyo. Kisha alienda nje na kulala kwenye nyasi akiwa pamoja na kaka zake.
“Karibu majira ya saa tatu asubuhi, mwanamume huyo, ambaye alionekana kuwa mzee na mgonjwa, alibebwa hadi ndani ya ua wa mahakama kwa baiskeli. Kwa kuzingatia hali yake, Afisa wa Kuwahudumia Wateja alimpa Kadi ya Kipaumbele,” ilisema Idara ya Mahakama kwenye taarifa iliyotumwa na msemaji wake Paul Ndemo.
Kadi hiyo hupewa wazee, wajawazito, walemavu na wagonjwa ili kesi zao zishughulikiwe haraka.
“Wakati afisa wa mahakama alipoenda kumpa taarifa zaidi, alibaini kuwa hakuitikia. Polisi waliitwa mara moja na ikabainika kuwa mwanamume huyo kwa bahati mbaya alikuwa amefariki.”
Kifo cha mwanamume huyo kinakuja wiki chache baada ya afisa mmoja wa polisi kufyatua risasi kimakosa na kuwajeruhi watu watano katika mahakama ya Bungoma.
