Mzaliwa wa Kenya Madina Okoth asajiliwa na Atlanta Dream

Okot alikuwa chaguo la 13 kwa jumla kati ya nafasi 15 za kwanza zilizopatikana

Marion Bosire
2 Min Read

Nyota wa mchezo wa mpira wa vikapu mzaliwa wa Kenya, Madina Okot, alichaguliwa na timu ya Atlanta Dream.

Haya yalifanyika katika raundi ya kwanza ya rasimu ya Shirikisho la Mpira wa Kikapu la Wanawake la Kitaifa, WNBA,  ya mwaka 2026 usiku wa Jumatatu.

Okot alikuwa chaguo la 13 kwa jumla kati ya nafasi 15 za kwanza zilizopatikana katika hafla iliyofanyika huko The Shed at Hudson Yards jijini New York.

“Nina furaha sana kuwa hapa leo. Kuchaguliwa tu, ni ndoto iliyotimia. Nina furaha sana kwamba nitaweza kushindana dhidi ya wachezaji bora ambao nimekuwa nikitazama na kuwaenzi tangu nikiwa mdogo,” alisema Okot akiwa na hisia kali.

Okot alizaliwa huko Mumias Magharibi mwa Kenya, lakini alianza kucheza voliboli akiwa shule ya upili ya Bishop Sulumeti huko Kakamega. Aliacha voliboli na kuingilia mpira wa kikapu alipohamia shule ya upili ya Kaya Tiwi.

Aliiwakilisha Kenya katika mpira wa kikapu wa wachezaji watatu kila upande kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola kabla ya kuichezea timu ya Kenya Ports Authority katika ligi ya Kenya ya mpira wa kikapu.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Mississippi kabla ya kuhamia Chuo Kikuu cha South Carolina. Safari ya Madina Okot kuelekea WNBA ilipitia timu ya chuo hicho katika NCAA, ambayo imetoa nyota wakubwa wa WNBA kama A’Ja Wilson.

Okot alitumia msimu mmoja tu na Gamecocks baada ya kujiunga na programu hiyo kwa msimu wa 2025/2026. Alionyesha kiwango bora katika mwaka wake wa mwisho, akipata heshima za kikosi cha pili cha All-SEC na kufika fainali ya tuzo ya Lisa Leslie Centre of the Year.

Alinyimwa mwaka mwingine katika NCAA na kulazimika kupanda ngazi, na kwa bahati nzuri Atlanta Dream walimchukua. Madina Okot sasa amejiunga rasmi na Atlanta Dream.
Okot sasa anaungana na Atlanta Dream, timu ambayo hivi karibuni ilimsajili mmoja wa nyota bora wa mchezo huo, Angel Reese.

Share This Article