Wanawake kote nchini wamehimizwa kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika kinyang’anyiro cha uongozi wa kisiasa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Wito huo ulitolewa katika Kijiji cha Mulukhoni, Kaunti Ndogo ya Samia, ambapo Balozi Josephine Ojiambo alihimiza wanawake kujitosa katika siasa na kuwania nafasi za uongozi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikihodhiwa na wanaume.
Akizungumza baada ya kukutana na wazee wa Samia kuomba baraka zao, Ojiambo alisema uwakilishi mkubwa wa wanawake katika uongozi utasaidia kubadilisha sura ya siasa nchini na kuendeleza masuala yanayohusu wananchi katika jamii.
Kwa mujibu wa Profesa Julia Ojiambo, binti yake yuko tayari kuchukua wadhifa wa uongozi na sasa amewageukia wazee wa Samia kuomba baraka zao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Lydia Nasubu, Naibu Mwenyekiti wa kundi la kina mama wa jamii ya Samia, yaani Samia Women Achievers Alliance, ambaye alitoa wito kwa wanawake zaidi kujitosa katika nafasi za uongozi na kutumia ushawishi wao kuendeleza maendeleo na kuwawezesha jamii.
Balozi Josephine Ojiambo anawania wadhifa wa ubunge huko Funyula katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.