Kenya yasisitiza umoja wa Afrika na diplomasia ya amani

Mudavadi alisema hayo katika kikao cha 26 cha Dharura cha Baraza la Utendaji la Umoja wa Afrika, AU, jijini Luanda, nchini Angola.

Marion Bosire
2 Min Read

Mkuu wa mawaziri ambaye pia ni waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi, amesisitiza tena dhamira ya Kenya ya kuimarisha umoja wa Afrika, ushirikiano wa kidiplomasia na amani kama nguzo muhimu za maendeleo ya bara hili.

Katika kikao cha 26 cha Dharura cha Baraza la Utendaji la Umoja wa Afrika, AU, jijini Luanda, nchini Angola, Mudavadi alijiunga na mawaziri wengine wa mambo ya nje wa Afrika, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la AU, Édouard Bizimana na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf.

Dhamira ya kikao hicho ikiwa kuendeleza suluhu zinazoongozwa na Afrika za kuzuia migogoro, kuimarisha mwitikio wa mapema na kukabiliana na vitisho vipya vya usalama.

Alisema Kenya inaunga mkono juhudi za kutimiza lengo la AU la kutokomeza silaha kufikia mwaka 2030 kupitia mazungumzo, diplomasia na taasisi imara zaidi.

Mudavadi alisisitiza kuwa amani pia ni hitaji la kiuchumi, kwani huwezesha mipaka salama, biashara imara, uwekezaji mkubwa na fursa zaidi kwa vijana wa Afrika.

Pembezoni mwa kikao hicho, Mudavadi alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sierra Leone, Mohamed Rahman Swaray, kuhusu kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili katika ushirikiano wa pande mbili na wa kimataifa.

Mudavadi pia alishukuru Sierra Leone kwa kumtunuku Luteni Jenerali Mstaafu Daniel Opande tuzo ya Grand Commander of the Order of the Rokel, kutambua mchango wake mkubwa kwa Sierra Leone katika kipindi muhimu cha historia ya nchi hiyo.

Waziri huyo alisema Kenya inatarajia kumkaribisha Rais wa Sierra Leone, Julius Maada Bio, jijini Nairobi mwezi Disemba kwa Mkutano wa Dharura wa AU kuhusu uzalishaji wa ndani wa bidhaa za dawa na bidhaa zisizo za dawa.

Share This Article