Mahakama Kuu imesimamisha kuanzishwa kwa matumizi ya Maisha Card, ambavyo ni vitambulisho vipya vya kidijitali vinavyotazamiwa kuanza kutumika nchini Kenya kuchukua nafasi ya vitambulisho vya zamani.
Jaji Lawrence Mumbi alipiga breki kuanza kutumika kwa vitambulisho hivyo hadi pale kesi iliyowasilishwa mahakamani kupinga matumizi yake itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Wanaharakati na watetezi wa haki walienda mahakamani kupinga hatua ya serikali ya kuwapa Wakenya wote wanaopoteza vitambulisho vya kitaifa Maisha Card kama njia ya kushinikiza matumizi yake.
Maisha Card itatumika kwa huduma kadhaa ikiwemo kitambulisho cha kitaifa, leseni ya kuendesha gari na taarifa muhimu za kila mwananchi badala ya sasa ambapo mwananchi huwa na vitambulisho kadhaa kila kimoja na utambulisho tofauti.
Kuanzishwa kwa matumizi ya vitambulisho hivyo vya Maisha Card vimekumbwa na pingamizi mahakamani mara kadhaa.