Jux akanusha madai ya kutelekeza mama na mtoto

Ameamua kufuata mkondo wa sheria kutatua suala hilo, akiahidi hatua za kisheria dhidi ya mhusika.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Juma Jux amekanusha madai yaliyoibuliwa hivi maajuzi mitandaoni kwamba ana mama na mtoto ambao ametelekeza nchini Tanzania.

Jux ambaye ameoa mwigizaji na mwanabiashara wa Nigeria Pricillia Ojo, anasema ameamua kuzungumza baada ya kutazama suala hilo kwa muda akiwa kimya.

Madai hayo anasema yamegusa jina lake, familia yake, biashara zake na nembo yake ambayo amekuwa akiijenga kwa miaka mingi.

Amefichua kwamba madai hayo yaliwahi kuibuka awali ambapo aliamua kutafuta mhusika kufahamu ukweli wa madai hayo. Mhusika huyo wakati huo alikiri kwamba hakuwahi kukutana naye kimwili wala kuwa na uhusiano wa kimapenzi naye.

Msanii huyo anasema aliombwa na mhusika kususia suala hilo kwani chanzo chake kilikuwa ni maoni ya baadhi ya mashabiki waliodai mtoto huyo anafanana na yeye, ndipo wakaanza kumhusisha naye.

Zamu hii Jux amesema kwamba ameamua kufuata mkondo wa sheria kutatua suala hilo, akiongeza kusema kwamba hatua zaidi zitachukuliwa dhidi ya mhusika.

Juma ameonya pia vyombo vya habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii dhidi ya kusambaza taarifa zinazoweza kupotosha umma bila kuhakikisha ukweli wake kwanza.

Ameonya kwamba yeyote atakayehusisha jina lake, familia yake au biashara zake na madai yasiyo ya kweli atawajibishwa kisheria na kwamba amechagua kutulia, kushikilia ukweli na kuacha suala hilo lifuate mkondo wa sheria.

Share This Article