Jose Chameleone ashauri mwanawe kuwa baba bora

Hii ni baada yake kugundua kwamba Abba Marcus na mpenzi wake wanatarajia mtoto.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii nguli wa muziki nchini Uganda Jose Chameleone amefichua ushauri aliompa mwanawe Abba Marcus baada ya kugundua kwamba anatarajia mtoto na mpenzi wake.

Akizungumza kwenye mahojiano ya kipindi cha NBS After 5, Chameleone alisema kwamba alifurahia sana kwani sasa yuko karibu kuitwa babu, hata ingawa Marcus ni mdogo sana kuanza familia, lakini akamshauri Abba kuwa baba bora kwa mwanawe mtarajiwa.

Chameleone pia alimshauri Marcus ambaye anajaribu kujiimarisha kama msanii wa muziki nchini Marekani, ampende mpenzi wake hasa wakati huu wa ujauzito na kuhakikisha kwamba anaweza kutimiza mahitaji ya familia yake changa.

Alipoulizwa iwapo yeye amekosa kutimiza mahitaji yake kama baba, Chameleone alisema kwamba hajakosa kufanya jukumu lake kama baba.

Katika mahojiano hayo, Chameleone alimzungumzia pia aliyekuwa mke wake na mama ya watoto wake Daniella Atim, akitambua kujitolea kwake walipokuwa pamoja na akamshukuru.

Alikumbuka uhusiano wao walipokuwa kwenye ndoa na anamshukuru kwa kumpa watoto watano na kusimama naye muda wote wa ndoa yao.

Kuhusu mjadala unaoendelea nchini Uganda wa vipimo wa DNA kwa watoto, Jose Chameleone alisema kwamba yeye hana sababu ya kutaka kufanya vipimo hivyo.

Mjadala huo unafuatia ufichuzi kwamba kati ya watoto 25 waliokuwa wakidai kuwa watoto wa marehemu mwanamuziki Paul Kafeero, ni wanne tu waliothibitishwa kuwa wanawe kupitia vipimo vya DNA.

Share This Article