Kundi la kutetea haki za binadamu limesema kuwa wanamgambo wa Sudan walifanya uhalifu dhidi ya ubinadamu na utakasaji wa kikabila wakati wa kampeni yao ya kuuteka mji wa El-Fasher mwaka jana.
Kuzingirwa na kutekwa kwa mji huo ulioko katika eneo la magharibi la Darfur kulikuwa miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya umwagaji damu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, vinavyopiganwa kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha Rapid Support Forces (RSF).
Katika ripoti ya uchunguzi iliyotolewa Jumatano, Amnesty International ilisema:
“Uhalifu uliofanywa na RSF ulijumuisha mauaji, kuwahamisha watu kwa nguvu, kuwafunga bila sababu za kisheria, mateso, ubakaji, utumwa wa kingono, aina nyingine za ukatili wa kingono, utumwa, mauaji ya halaiki, na mateso kwa misingi ya utambulisho.”
RSF haijasema chochote kuhusu ripoti hiyo ya Amnesty, lakini hapo awali ilikanusha tuhuma kama hizo.
Sudan bado imo katika mapambano ya madaraka yaliyodumu kwa miaka mitatu kati ya jeshi la kawaida la nchi hiyo na wanamgambo wa RSF. Vita hivyo vimeua mamia ya maelfu ya watu na kuwalazimisha zaidi ya watu milioni 14 kuyakimbia makazi yao.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ukatili wa kingono dhidi ya wanaume, wanawake na watoto unatumiwa kama silaha ya vita.
Pande zote mbili, RSF na Sudanese Armed Forces (SAF) zimeshutumiwa kwa kufanya uhalifu wa kivita, ingawa zote zimekanusha tuhuma hizo.
Baada ya kufukuzwa kutoka mji mkuu, Khartoum, mwezi Machi mwaka jana, RSF ilielekeza nguvu zake katika kuimarisha udhibiti wake wa eneo la magharibi la Darfur kwa kuuteka mji wa El Fasher, pamoja na kupanua ushawishi wake katika majimbo ya Kordofan yaliyoko kusini mwa nchi.
Taarifa ya BBC