Idara ya Mahakama nchini Zambia imetangaza kwamba ombi la kupinga uchaguzi wa Urais wa Agosti 13, 2026, limewasilishwa kwayo.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, naibu mkurugenzi wa mawasiliano ya umma katika idara hiyo Kalumba Chisambisha-Slavin, alithibitisha kupokelewa kwa ombi hilo kwa njia ya la kielektroniki.
Kalumba alifafanua kwamba hati hiyo ilitumwa kwenye anwani ya barua pepe ya kibinafsi ya Jaji Mkuu, Dkt. Mumba Malila.
Mawasiliano hayo yalitoka kwa mwananchi na yalikuwa na nyaraka zilizoelezwa kama “ombi la wananchi la uchaguzi wa rais,” pamoja na nyaraka nyingine zinazohusiana.
Mahakama imesema inafahamu madai yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii kwamba ombi hilo tayari limewasilishwa rasmi na kwa utaratibu unaostahili.
Hata hivyo, Mahakama ilieleza kuwa njia iliyotumika kuwasilisha nyaraka hizo sio ya kawaida sana lakini licha ya hali hiyo, Jaji Mkuu, akitumia mamlaka yake ya kiutawala, amewasilisha nyaraka hizo kwa Mahakama ya Katiba ili zizingatiwe.
Hatua hiyo inalenga kuiwezesha Mahakama kuamua iwapo ombi hilo liliwasilishwa kwa usahihi, huku idara ya Mahakama ikishauri wahusika kusubiri taarifa kutoka Mahakama ya Katiba kuhusu suala hilo.
Mwasilishaji wa ombi hilo huenda aliamua kutumia njia hiyo ya barua pepe kutokana na hatua ya serikali ya kufunga vituo vya mahakama Jumatatu Agosti 24, 2026 hatua iliyochukuliwa kuwa ya kuzuia uwasilishaji wa maombi ya kupinga uchaguzi wa Urais.