Asige aanzisha mpango wa kuhakikisha ulinzi imara wa kisheria kwa walemavu

Amechochewa na taarifa za ukiukaji wa haki za walemavu, licha ya kupitishwa kwa Sheria ya Walemavu ya mwaka 2025.

Marion Bosire
2 Min Read

Seneta Mteule Crystal Asige amezindua mpango mpya unaolenga kuimarisha upatikanaji wa haki kwa walemavu.

Kiongozi huyo amechochewa na kuendelea kupokelewa kwa taarifa za ukiukaji wa haki za walemavu, licha ya kupitishwa kwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2025.

Asige amesema afisi yake inaweka msingi wa mfumo endelevu wa msaada wa kisheria utakaoboreshwa kwa kuimarisha huduma za msaada wa kisheria, kuanzisha njia za rufaa, kusaidia mashauri ya kimkakati, kujenga uwezo wa mawakili, na kuhamasisha umma kuhusu haki za kisheria.

Mpango huo pia unajumuisha kuanzishwa kwa kliniki maalum za msaada wa kisheria na programu bunifu za kuwafikia wananchi ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaweza kutetea na kudai haki zao ipasavyo.

Seneta huyo ameshukuru Chama cha Wanasheria Nchini, LSK kwa kushirikiana naye katika mpango huo, akisema ushirikiano huo ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji kamili wa sheria mpya na kuhakikisha hakuna mtu mwenye ulemavu anayeachwa nyuma.

Sheria mpya ya Watu Wenye Ulemavu nchini Kenya, yaani Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2025, ilisainiwa na kuwa sheria tarehe 8 Mei 2025, ikichukua nafasi ya Sheria ya mwaka 2003.

Seneta Mteule Crystal Asige alikuwa mdhamini mkuu na mtetezi wa mfumo huo wa kisheria tangu hatua za kuandaliwa kwake kama mswada hadi kupitishwa kwake na kutiwa saini.

Share This Article