Mahakama Kuu ya Kisumu imewapata kaka wawili na hati ya kuua bila kukusudia, na kuwahukumu kifungo cha miaka 14 gerezani kila mmoja.
Dayon Okello Ochieng mwenye umri wa miaka 25 na Emmanuel Opiyo Ochieng mwenye umri wa miaka 21, walipatikana na hatia ya kumuua Charles Ogweno Ogolla Mei 27 2024, katika kijiji cha Dirubi, kata ndogo ya Siany, kaunti ndogo ya Nyakach, kaunti ya Kisumu.
Awali wawili hao walikuwa wamekanusha mashtaka hayo, lakini baada ya majadiliano na upande wa mashtaka, walikiri kumuua mwalimu huyo.
Wawili hao wanadaiwa kutekeleza mauaji hayo, baada ya kudaiwa kuwa mwathiriwa alikuwa akishiriki uchawi, hatua iliyosababsha ndugu hao kumshamulia kwa vifaa butu na kumuua.
Akitoa hukumu hiyo, Justice Joe Omido, alidokeza kuwa Ogolla alikuwa tegemeo kwa familia yake, na kifo hicho kimewanyima watoto wake utunzi wa mzazi, na kusababisha changamoto ya kiuchumi na kijamii.
“Ghasia haziwezi kubaliwa kuwa njia ya kusuluhisha mizozo ya kifamilia,” alisema Jaji huyo.
Wawili hao wamepewa siku 14 kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.