Mabadiliko ya kidijitali muhimu kwa vita dhidi ya ufisadi, yasema EACC

Martin Mwanje
2 Min Read
Abdi Mohamud - Mkurugenzi Mtendaji wa EACC

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini, EACC sasa inatoa wito kwa taasisi za sekta ya haki nchini kukumbatia mabadiliko ya kidigitali ili kusaidia kuimarisha mapambano dhidi ya jinalizi la ufisadi nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Abdi Mohamud ametaja mabadiliko ya kidijitali kuwa chombo cha kimkakati katika kuhamasisha uwazi, uwajibikaji na vita dhidi ya ufisadi nchini.

“Teknolojia sasa ni mwezeshaji mkubwa katika uzuiaji wa ufisadi, utekelezaji wa sheria na uwazi. Kwa taasisi za sekta ya haki, mifumo salama ya dijitali haipaswi kuwa chaguo, bali kipengele muhimu katika utendaji kazi wetu wa kila seiku,” alisema Mohamud.

Aliyasema hayo wakati wa mazungumzo ya ngazi ya juu ya jopo kwenye Mkutano wa 38 wa Baraza la Kitaifa la Utawala wa Haki, NCAJ uliofanyika jijini Mombasa leo Jumatatu.

Kulingana naye, mabadiliko ya kidijitali yanatoa fursa ya kipekee ya kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi serikalini katika kuzuia, kutambua, kuchunguza na kuwashtaki washukiwa wa ufisadi.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Martha Koome alisisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa taasisi za sekta ya haki, akisema umma unatumia mfumo wa haki kwa mtazamo wa kitu kimoja.

“Pamoja, kupitia kwa NCAJ, ni lazima twendelee kuimarisha imani ya umma katika utawala wa sheria, kuboresha upatikanaji wa haki na kujenga mfumo wa sheria ambao kwa kweli unatoa kipaumbele kwa watu,” alisema Jaji Koome.

 

Share This Article