Mgomo uliopangwa kufanywa na wafanyakazi wa usafiri wa anga sasa umesitishwa kwa kipindi cha mwezi mmoja ujao.
Hii ni baada ya serikali, kupitia kwa Katibu wa Usafiri wa Anga Teresia Mbaika, kuingilia kati na kuepusha mgomo huo ambao ulitazamiwa kutatiza usafiri wa anga kwa kiwango kikubwa.
Makubaliano ya kusitisha mgomo huo yalifikiwa leo Jumatatu katika mkutano uliohudhuriwa na Mbaika na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Usafiri wa Anga nchini (KAWU) Moss Ndiema miongoni mwa maafisa wengine.
Wakati wa mkutano huo, pande zote zilikubaliana kufanya msururu wa mikutano ili kusuluhisha matatizo yanayokumba taasisi mbalimbali katika sekta hiyo.

Mazungumzo yanayoihusisha kampuni ya Kenya Airways (KQ) na kampuni tanzu ya Jambojet yamepangwa kufanyika kesho Jumanne, Julai 28. Hata hivyo, mazungumzo hayo hayataangazia mzozo wa utambuzi wa Jambojet ambao kwa sasa ni suala linalotarajiwa kusuluhishwa na Mahakama ya Kutatua Mizozo ya Wafanyakazi, ELRC.
Masuala yanayofungamana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (KAA) yatajadiliwa keshokutwa Jumatano.