Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse ameimarisha kampeni ya kumtafutia Rais William Ruto uungwaji mkono katika eneo la Ukambani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Mutuse, anayefahamika mno kwa kuwasilisha hoja ya kumtimua Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua bungeni, ameonya kuwa eneo hilo halitaambulia chochote ikiwa litasalia katika upinzani.
Kulingana naye, kufanya kazi na serikali kutasaidia kuharakisha kasi ya maendeleo katika eneo la Ukambani ambalo kwa kawaida limemshabikia kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa miaka na mikaka.
Kalonzo anamezea mate kiti cha uraisa katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza wakati wa mpango wa uwezeshaji wanawake kiuchumi katika soko la Kee, wadi ya Kee katika eneo bunge la Kaiti, Mutuse ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kiukiunga mkono chama cha UDA akilalama kuwa eneo hilo limeonja machungu ya upinzani kwa muda mrefu mno.