Ruto ataka biashara EAC kuongezwa hadi asilimia 50

Alitoa wito huo Julai 27 alipokutana na Katibu Mkuu wa EAC Stephen Mbundi katika Ikulu ya Nairobi. 

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto ametoa wito kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwa mstari wa mbele katika kuongeza kiwango cha biashara kati ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo. 

Amesema kiwango cha biashara kati ya nchi wanachama bado kipo chini ilhali kinaweza kuboreshwa ikiwa hatua madhubuti zitachukuliwa.

“Kama jumuiya ya kikanda iliyopiga hatua zaidi barani Afrika, biashara kati ya nchi wanachama wa EAC ni takriban asilimia 20 ilhali inaweza kuongezwa hadi ikafikia asilimia 50 ikiwa hatua za kimkakati zitachukuliwa,” alisema Rais Ruto.

Aliyasema hayo leo Jumatatu alipokutana na Katibu Mkuu wa EAC Stephen Mbundi katika Ikulu ya Nairobi.

“Tulisisitiza wajibu wa EAC kama mwezeshaji mkuu wa maendeleo ya kikanda kupitia ulinganishaji wa ushuru wa forodha, ambao utaongeza biashara, kubuni nafasi za ajira, na kuchochea ustawi wa raia wote wa Afrika Mashariki,” aliongeza Ruto.

Wakati wa mkutano huo, viongozi hao waliangazia hatua inayopigwa na EAC, ikiwa ni pamoja na kuongeza utangamano miongoni mwa nchi wanachama, biashara ya kikanda na usafiri wa watu.

Share This Article