Watu watatu wamenusurika kifo kwa tundu la sindano baada ya lori lao aina ya Canter kugongwa na treni katika kivuko cha reli cha Limuru.
Dereva wa lori hilo amesema kuwa mwendeshaji wa treni hakupiga honi kuwaonya madereva waliokuwa wakivuka reli.
Alidai kuwa treni hiyo ilikuwa ikirudi nyuma kutoka upande wa Nakuru huku hali ya hewa ikiwa na ukungu mzito, jambo lililopunguza uwezo wa kuona.
Sasa wakazi na watumiaji wa barabara wanalitaka Shirika la Reli la Kenya kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Kiambu kutafuta suluhisho la kudumu katika eneo hilo.
Wanasema kizuizi cha reli kilichokuwa kimewekwa awali kilisaidia kudhibiti mtiririko wa magari na kuimarisha usalama katika kivuko hicho.
Taarifa ya Marion Bosire na Ephantus Githua