Ujenzi wa Chuo cha Kilimo kukamilika kufikia Disemba, asema Katibu Ronoh

radiotaifa
1 Min Read
Katibu Dkt. Kipronoh Ronoh (aliyevalia shati jeupe) wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Chuo cha Kilimo cha Kenya huko Tigania Magharibi

Katibu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh amewahakikishia wakazi wa eneo bunge la Tigania Magharibi kuwa ujenzi wa Chuo cha Kilimo cha Kenya (KSA) unaoendelea katika eneo la Kamutune utakamilika kufikia mwezi Disemba mwaka huu. 

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika eneo bunge hilo, Dkt. Ronoh alisema serikali imeimarisha juhudi za kuharakisha ujenzi wa chuo hicho kwa lengo la kuhakikisha kinaanza kuhudumu kama ilivyoratibiwa. ‎

Pia alikagua ujenzi unaoendelea wa vituo mbalimbali vya uzalishaji wa kilimo katika maeneo ya Urru na Ngundune.

‎Ronoh alidokeza kuwa serikali ya Kenya Kwanza ikiongozwa na Rais William Ruto bado inadhamiria kutimiza ahadi zote ilizotoa kwa Wakenya kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ulioharakishwa.

Alitoa wito kwa wakazi kuwekeza katika nyumba za makazi watakamoishi wanafunzi, wakufunzi na wafanyakazi wengine punde chuo hicho kitakapoanza kuhudumu. ‎

Chuo cha Kilimo cha Kenya kinatazamiwa kuwapa wahitimu ujuzi wa hali ya juu kiasi cha kuboresha huduma za kilimo za nyanjani na kuboresha uzalishaji mashambani siyo tu katika eneo la Tigania Magharibi bali pia nchini kote.

Taarifa ya Dickson Mwiti 

Share This Article