Wetang’ula tosha 2032, wasema viongozi wa Bonde la Ufa

Viongozi hao wamesifia uongozi wa Wetang'ula wa shughuli za bunge na mchango wa Seneta huyo wa zamani wa Bungoma katika ushindi wa Rais Ruto mwaka 2022.

Martin Mwanje
2 Min Read
Spika Moses Wetang'ula na viongozi wengine katika hafla ya kuchangisha pesa eneo la Aldai, kaunti ya Nandi

Baadhi ya viongozi wa Bonde la Ufa wamemuunga mkono Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula kuchukua hatamu za kuongoza nchi hii baada ya Rais William Ruto kuondoka madarakani. 

Viongozi hao, wakiongozwa na Gavana wa kaunti ya Nandi Stephen Sang, wamesema Wetang’ula ndiye anayefaa zaidi kumrithi Rais Ruto mwaka 2032.

Nao walitoa tangazo hilo wakati wa hafla ya kuchangisha fedha katika eneo bunge la Aldai, kaunti ya Nandi.

Kulingana nao, tangazo lao ni utambuzi wa mchango wa Wetang’ula katika ushindi wa Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 na kuendelea kwake kuunga mkono utawala wa Kenya Kwanza.

Pia walitambua mchango unaofanywa na jamii wa Waluhyia katika kuunga mkono uongozi wa Rais Ruto.

Gavana Sang alisema mchango wa Wetang’ula kwa Rais Ruto kuchukua urais wa nchi utasalia kuwa sura muhimu katika historia ya siasa za nchi hii.

“Simulizi ya ushindi wa Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 haiwezi kusimuliwa bila kutambua wajibu uliotekelezwa na Wetang’ula. Mchango wake ni sehemu ya historia ya siasa ya Kenya, na tunatambua mchango aliotupta,” alisema Sang.

Aliongeza kuwa eneo la Bonde la Ufa litamuunga mkono Wetang’ula kumrithi Rais Ruto punde atakapomaliza muhula wake wa pili mwaka 2032.

Wito sawia ulitolewa na mbunge wa Tinderet Julius Melly aliyesema Wetang’ula amedhihirisha uongozi, uzoefu na ushujaa wa kitaifa unaohitajika kuongoza nchi, akitoa mfano wa usimamizi wake wa shughuli za bunge.

Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Vihiga Beatrice Adagala ni miongoni mwa waliounga mkono kauli hiyo wakimtaja Wetang’ula kuwa kiongozi mwenye maono na mwonekano wa kitaifa unaohitajika kuiongoza nchi.

Baadhi ya viongozi wa eneo la Pwani wamesikika wakimpigia debe Waziri wa Madini Hassan Joho kumrithi Rais Ruto baada ya uongozi wake kukamilika.

Ilivyo, idadi ya wanaomezea mate kiti chas urais itaongezeka zaidi hasa mwaka 2032.

Share This Article