Ruwaza 2030 haijatimiza malengo yake kikamilifu, asema Rais Ruto

Rais Ruto alithibitisha kuwa taifa hili limekosa kutimiza baadhi ya malengo yake kwenye ruwaza hiyo.

Tom Mathinji
1 Min Read
William Ruto - Rais wa Kenya.

Rais William Ruto amesema ruwaza ya mwaka 2030 imekosa kutimiza malengo yake kikamilifu, huku muda wake wa kutekelezwa ukikaribia kukamilika.

Kiongozi wa taifa alidokeza kuwa ruwaza ya mwaka 2030 imeongoza ajenda ya Kenya kwa muda wa miongo miwili, lakini akakiri kuwa baadhi ya malengo yake bado hayajatimizwa kikamilifu.

“Kwa muda wa miongo miwili, ruwaza 2030 ilielekeza maendeleo ya taifa, sera za umma na kuchochea kuzinduliwa kwa katiba mpya,” alisema Rais Ruto.

Huku akiisifu ruwaza hiyo, Ruto alisema ruwaza hiyo ilibadilisha jinsi Kenya ilivyotekeleza maendeleo ya taifa kwa kutoa mwelekeo mwafaka wa uwekezaji, sera za taifa na mipango ya muda mrefu.

“Ilihudumia Kenya vyema. Ilibadilisha mtazamo wetu kuhusu maendeleo ya taifa na kutoa mwelekeo mwafaka na nguvu iliyopo kwenye mipango ya muda mrefu,” alidokeza Rais Ruto.

Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, Ruto alithibitisha kuwa taifa hili limekosa kutimiza baadhi ya malengo yake kwenye ruwaza hiyo.

“Ruwaza ya mwaka 2030, iliweka malengo ya taifa hili ya kuwa uchumi ulioimarika wa kiwango cha kadri kufikia mwaka 2030, lakini hayo hayajatimzwa,” aliongeza kiongozi huyo wa taifa.

Aliyasema hayo Alhamisi usiku kwenye hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni.

Share This Article