Kenya yaungana na ulimwengu kuadhimisha siku ya Malaria duniani

Tom Mathinji
1 Min Read
Kenya yajiunga na ulimwengu kuadhimisha siku ya Malaria duniani.

Kenya imeungana na dunia leo Aprili 25,2026 kuadhimisha siku ya Malaria duniani, huku miito ikitolewa ya kuangamiza ugonjwa huo duniani.

Maadhimisho hayo yanajiri huku taifa hilo la Afrika ya Mashariki likisambaza vyandarua vya kuzuia mbu milioni 10 kwa lengo la kuimarisha uhamasishaji wa umma dhidi ya ugonjwa huo.

Usambazaji huo wa vyandarua utanza katika kaunti za Baringo, Busia, Kakamega na Siaya, kabla ya kupanuliwa katika kaunti zingine.

Mpango huo unalenga kuafikia lengo la kupunguza Malaria kwa asilimia 80 na kupunguza maafa yanayotokana na Malaria kwa asilimia 90.

Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni, alisema Kenya imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na ugonjwa wa Malaria ambapo visa vya ugonjwa huo vilipungua kwa asilimia 5 kati ya mwaka 2023 na 2025, na vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo kupungua kwa asilimia 32.

Takriban watu billioni 3.3 kutoka mataifa 106 ya dunia wako katika hatari ya kuugua ugonjwa wa malaria.

Shirika la Afya Duniani (WHO), limetangaza nchi 47 duniani kuwa zimeangamiza ugonjwa wa Malaria, huku nchi 25 zikianzisha chanjo dhid ya Malaria ili kuwalinda watoto milioni 10 kila mwaka.

Nchini Kenya, maadhimisho ya mwaka huu yanatekelezwa katika shule ya msingi ya Rukenya kaunti ya Kirinyaga.

Share This Article