Papa Leo ashushia rungu mataifa tajiri na “madikteta” wanaochochea vita

KBC Digital News
2 Min Read
Papa Leo

Papa Leo ametoa maneno makali na ya nadra dhidi ya viongozi wanaotumia mabilioni ya dola kufadhili vita, akisema kuwa dunia kwa sasa “inaharibiwa na kundi dogo la madikteta.”

Kauli hizo nzito alizitoa akiwa ziarani nchini Cameroon, ikiwa ni siku chache tu tangu Rais wa Marekani, Donald Trump, alipomshambulia kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki kupitia mitandao ya kijamii.

Papa Leo, ambaye anaweka historia kama Papa wa kwanza kutoka nchini Marekani, pia amewakemea vikali viongozi wanaotumia lugha za kidini kuhalalisha mapigano.

Akiwa katika jiji kubwa zaidi kwenye kanda zinazozungumza Kiingereza nchini Cameroon – eneo ambalo limegubikwa na mgogoro wa muda mrefu uliopoteza maisha ya maelfu ya watu – aliwataka viongozi hao kufanya “mabadiliko ya haraka na ya dhati” ya mwelekeo wao.

“Mabwana wa vita wanajifanya kutojua kuwa inachukua sekunde moja tu kubomoa, lakini maisha ya mwanadamu mara nyingi hayatoshi kujenga upya kile kilichoharibiwa,” alisisitiza kiongozi huyo.

Aliongeza kuwa viongozi hao wanajifanya hawaoni jinsi mabilioni ya dola yanavyomwagwa kwenye mauaji na uharibifu, huku rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya matibabu, elimu, na kurejesha matumaini zikiwa hazipatikani popote.

Mashambulizi ya maneno ya Trump dhidi ya Papa Leo, yaliyoanza usiku wa kuamkia ziara yake kubwa katika nchi nne za Afrika na kurudiwa tena Jumanne usiku, yamezua taharuki na masikitiko makubwa barani Afrika. Ikumbukwe kuwa zaidi ya asilimia 20 ya Wakatoliki wote duniani wanaishi barani humu.

Papa Leo, ambaye katika mwaka wake wa kwanza wa uongozi wa kanisa lenye waumini bilioni 1.4 alikuwa mtulivu na asiyependa makuu, sasa ameibuka kuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa vita vilivyoanza kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran.

Share This Article