Wawakilishi wa Marekani na Iran wanashiriki meza ya mazungumzo nchini Pakistan kwa lengo la kufufua juhudi za amani kati ya nchi hizo mbili, baada ya wiki nane za mvutano mkubwa wa kijeshi.
Hata hivyo, Iran imesema maafisa wake hawako tayari kukutana na wawakilishi hao wa Marekani kwa mashauriano ya kumaliza vita, ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuvuruga biashara katika masoko ya kimataifa.
Ikulu ya White House imesema mjumbe maalum wa Rais Donald Trump Steve Witkoff na mkwewe wa kiume Jared Kushner, wanatarajiwa kuondoka nchini humo kwenda kushauriana na waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Iran Abbas Araqchi.
Waziri wa ulinzi wa Marekani Pete Hegseth aliwaambia waandishi wa habari kwamba Iran ilikuwa na nafasi ya kutia saini mkataba mzuri na Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi aliwasili katika jiji kuu Islamabad siku ya Ijumaa.
Marekani na Iran zinaendeleza mzozo wa gharama kubwa huku Iran ikifunga eneo la bahari la hormuz, ambalo hutumika katika safari za meli za usafirishaji mafuta, ilhali Marekani inazuia usafirishaji wa mafuta ya Iran.
Mzozo huo unaoingia wiki ya tisa umesababisha bei ya nishati kupanda, mfumuko wa bei ya bidhaa na hatari kwa ukuaji wa kimataifa.