Ni afueni kubwa baada ya Madaktari katika hospitali ya maalum ya watoto ya King Abdullah mjini Riyadh,Saudi Arabia, kufanikiwa kuwatenganisha pacha walioshikana wa Tanzania, Nancy na Nice.
Upasuaji huo uliochukua saa 16 na ambao ulikisiwa kuwa na ufanisi wa asilimia 60, ulianza siku ya Alhamisi ulifanywa na madaktari 35, wakiongozwa na Daktari Mkuu Dkt.Abdullah Al Rabeeah.
Dkt. Al Rabeeah, amesema kuwa pacha hao wenye umri wa miaka miwili walikuwa wameunganishwa chini ya kifua,katika tumbo,na nyonga huku wakitumia kwa pamoja viungo vya ini na utumbo.

Aidha, kulingana na Dkt.Al Rabeeah, Nancy na Nice, walitumia kibofu na kizazi kimoja na kila mmoja alikuwa na mguu mmoja huku wakigawana mguu mwingine mmoja na mguu mmoja wa mwisho ulikuwa umelemaa.
Upasuaji huo ulikuwa wa tatu kuhusisha pacha wa sampuli hiyo kutoka Tanzania na wa 71, kufanywa na hospitali hiyo chini ya mpango wa Saudi Conjoined Twins Program (SCT), ulioanzishwa miaka 35 iliyopita.
Pacha hao walizaliwa mwaka 2024.

Mama yao Angerine Magori, alijawa na furaha tele na shukran si haba, baada ya kukamilika kwa upasuaji huo mapema Ijumaa.