Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua ameapa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliodumisha kutimuliwa kwake madarakani.
Ametaja uamuzi huo kuwa wa kushangaza kwani licha ya kubaini kuwa Seneti haikumpa fursa ya kujitetea, Majaji hawakufutilia mbali hatua ya bunge hilo kumbandua madarakani.
“Haki ya kusikilizwa imekandamizwa na kupuuzwa mchana peupe. Tutawasilisha rufaa katika Mahakama ya Rufaa kuhusiana na uamuzi huo na kutumai tutatendewa haki,” alisema Gachagua aliyeandamana na Naibu kiongozi wa chama cha DCP Cleophas Malala na Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Kirinyaga Njeri Maina miongoni mwa viongozi wengine.
Njeri ni mmoja wa mawakili waliomwakilisha kwenye kesi ya kupinga kutimuliwa kwake.
“Shilingi milioni 50 nilizopewa na mahakama ni fedheha kwa haki zangu za kimsingi na uhuru na dhihaka kwa Katiba.”
Kwenye uamuzi huo, Majaji Erick Ogola, Freda Mugambi na Antony Mrima waliliagiza Bunge la Seneti kumlipa Gachagua fidia ya shilingi milioni 50 kwa kukosa kumpa fursa ya kusikilizwa wakati wa vikao vya kubanduliwa kwake.
Kwenye taarifa, Spika wa Seneti Amason Kingi amesema wanadhamiria kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.