Kampeni ya kitaifa ya kuchanja mifugo imezinduliwa rasmi katika wadi ya Segera, kaunti ya Laikipia.
Akiongoza uzinduzi huo leo Alhamisi, waziri wa kilimo na ustawi wa mifugo Mutahi Kagwe, alisema hatua hiyo inalenga kulinda mifugo dhidi ya magonjwa kama vile ule wa miguu na midomo.
Kulingana na waziri huyo, kampeni hiyo itakayotekelezwa katika muda wa miaka mitatu, itakuwa ya hiari na inawiana na mikakati ya kitaifa ya kudhibiti magonjwa dhidi ya mifugo.
Kupitia kampeni hiyo, waziri Kagwe alisema serikali inanuia kutokomeza ugonjwa wa miguu na mdomo na ule wa PPR, ambayo ni hatari kwa mbuzi, kondoo na ng’ombe. Magonjwa hayo kulingana waziri huyo, husababisha hasara katika uzalishaji na pia husambaratisha uchumi, kwa kusababisha hasara ya hadi shilingi bilioni 62.
“Serikali ya taifa na zile za kaunti, zimeshirikiana kuhakikisha magonjwa hayo yanatokomezwa kupitia mfumo ulioidhinishwa kimataifa kupitia Shirika la Afya ya mifugo Duniani (WOAH),” alisema Kagwe.
Alitoa wito kwa wakulima kutoa mifugo wao wachanjwe, akielezea ushirikiano wa pamoja kuimarisha uzalishaji na kulinda maisha.
Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Gavana wa Laikipia Joshua Irungu, katibu katika idara ya ustawi wa mifugo Jonathan Mueke na Mkurugenzi wa huduma za matibabu ya mifugo Dkt. Allan Azegele miongoni mwa wengine.