Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC imewakamata washukiwa 9 kutoka Wizara ya Fedha kama sehemu ya uchunguzi wa madai ya ulaghai wa shilingi bilioni 1.57.
Washukiwa hao wanazuiliwa katika makao makuu ya EACC jijini Nairobi wakisubiri kufikishwa mahakamani kesho Jumatano, Agosti 19.
9 hao walikamatwa kuhusiana na madai ya ufujaji na usambazaji wa kiulaghai wa shilingi bilioni 1.57 chini ya Mpango wa Upelekaji Mashinani wa Uvumbuzi na Teknolojia (PROFIT) unaotekelezwa na Wizara ya Fedha kwa ufadhili kutoka kwa Mfuko wa Kimataifa wa Ustawi wa Kilimo (IFAD).
“Uchunguzi wa EACC ulibaini kuwa shilingi bilioni 1.57 zilizambazwa kiulaghai kutoka Akaunti ya Ustawi ya Wizara ya Fedha hadi mpango wa PROFIT na kisha kusambazwa kwa taasisi 23 za kibinafsi, majina 15 ya biashara na kampuni nane, kwa bidhaa na huduma ambazo kamwe hazikutolewa,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo kwenye taarifa.
“Isitoshe, uchunguzi ulibaini kuwa maafisa wa mpango huo walitumia nyaraka bandia na za kughushi kuwajibikia fedha hizo na kufungua akaunti ya benki isiyoidhinishwa katika Benki ya KCB kwa jina la mpango wa PROFIT, ambapo kupitia kwake zilipokelewa na kubadhiriwa, huku kiasi kikubwa cha pesa taslimu kikitolewa.”
Washukiwa tisa waliokamatwa leo Jumanne ni John Ngure Kabutha, Namwel Moturi Motanya, John Maina Muriithi, Gladys Juliet Oroni alias Gladys Juliet, Brian Kiprop Chepkarat na Ian Kwemoi Chepkarat.
Wengine ni Josephat Kamau Kamoshe, James Omwondo Ndai, na Jimmy Carter Odoyo Osodo.
Wengine ambao wametakiwa kufika katika makao makuu ya EACC jijini Nairobi kuhusiana na sakata hiyo ni Billy Otieno Obango, Auma Ritah Otieno, Paul Mukasiali Shilaho, Susan Wangari Gathiaka na Erick Otieno Achila.
Miriam Roseline Obinda, Brown Mujenyi Agade, hilda Ndinda Ngava, Charles Cheruiyot na Jackline Kagai Saisi pia wametakiwa kufika EACC.