Wimbo ‘Beautiful’ wa Harmonize waondolewa YouTube

Uongozi wake ulieleza kuwa ni kutokana na madai ya hakimiliki kutoka kwa mtu fulani.

Marion Bosire
1 Min Read

Msanii wa Bongo Flava kutoka Tanzania, Harmonize, amejipata kwenye mzozo wa hakimiliki baada ya wimbo wake mpya, “Beautiful,” kuondolewa YouTube siku chache tu baada ya kutolewa.

Wimbo huo, uliotolewa Agosti 14, 2026, ulizinduliwa kama wimbo mkuu wa albamu yake ijayo, 31.

Hata hivyo, leo Agosti 18, wimbo huo umeondolewa kwenye jukwaa la video kufuatia kile ambacho uongozi wake ulieleza kuwa madai ya hakimiliki kutoka kwa mtu fulani.

Uongozi wa Harmonize, KondeGang, ulithibitisha kuondolewa kwa wimbo huo na kusema unashughulika kutatua mzozo huo. Hata hivyo, taarifa hiyo haikutaja hadharani mtu au kampuni iliyowasilisha dai hilo la hivi karibuni.

Tukio hilo linaongeza sura nyingine katika historia ya Harmonize ya kukumbana na malalamiko ya hakimiliki, huku baadhi ya nyimbo zake zilizopita zikiondolewa au kuzuiwa kwenye YouTube.

Miongoni mwa matukio yaliyojulikana zaidi ni kuhusu wimbo “Uno” wa mwaka 2019.

Mtayarishaji wa muziki kutoka Kenya, Magix Enga, alimtuhumu Harmonize kwa kutumia midundo kutoka kwenye wimbo wake aliomshirikisha King Kaka, “Dundaing,” bila kupata ruhusa.

YouTube baadaye iliiondoa nyimbo hiyo kufuatia dai la hakimiliki, huku usimamizi waa Harmonize ukifanya mazungumzo na Enga, na hatimaye wimbo huo ukarejeshwa kwenye YouTube.

Share This Article