Msanii wa muziki wa humu nchini Savara Mudigi amefichua kwamba alishapokea malipo ya kutumbuiza kwenye fainali za CHAN humu nchini mwaka jana.
Alisema haya alipokuwa akizungumza na wanahabari katka uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam nchini Tanzania jana muda mfupi baada ya kuwasili humo.
Mwanahabari mmoja alitaka kufahamu iwapo suala la malipo ya CHAN lilitatuliwa ikikumbukwa kwamba Zuchu ambaye ni msanii wa muziki kutoka Tanzania alihusishwa katika tumbuizo hilo na alilalamika kwamba hakuwa amelipwa.
Lakini Savara amejibu hilo akisema kwamba mara nyingi yeye huwa hashughuliki na masuala ya malipo kwani usimamizi wake ndio hushughulikia.
“Suala la kulipwa au kutolipwa ni usimamizi wangu unashughulikia, mimi ninashughulika na sanaa,” alisema msanii huyo ambaye ni mmoja wa wanachama wa kundi la muziki la Sauti Sol akibainisha kwamba malipo husika yalishakamilishwa.
Alipoulizwa kuhusu wimbo unaovuma kwa sasa wa Fainali wa Bien Barasa na Ali Kiba, Savara alionekana mwenye furaha akisema ni kazi nzuri na kwamba hata yeye mwenyewe alihusika katika maandalizi ya kazi hiyo.
“Ninafurahi sana kuona muziki wa Afrika Mashariki umeanza kusukuma na ndio maana niko hapa, ndugu yangu aliniambia ni lazima tuachilie video moto sana kwa sababu lazima uwashe moto.” Aliongeza Savara.
Savara yuko nchini Tanzania kwa ajili ya kuandaa wimbo wa pamoja na Barnaba Classic ambaye alimpokea jana katika uwanja wa ndege.