Wanachama watatu wa kundi la Fighting Brutality & Impunity (FBI) ambao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya ugaidi katika Mahakama ya Kahawa, wameondolewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ukitaja ukosefu wa ushahidi wa kutosha.
Kesi hiyo ambayo iliwasilishwa Septemba 29,2025, iliondolewa rasmi mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi Gideon Kiage, na hivyo kuhitimisha swala hilo.
Watatu hao Patrick Osoi, almaarufu The 6th, Jackson Kuria, almaarufu Cop Shakur, na Hiram Kimathi, wanaohusishwa na kundi hilo, walishtakiwa kwa kuvalia magwanda yanayofanana na yale ya kijeshi kuambatana na sehemu ya 184(1) ya katiba.
Kulingana na mashtaka dhidi yao, mnamo Juni 25,2025 Chama cha Kitaifa cha Wamiliki Bunduki (NGAO) cha ulengaji shabaha cha Kirigiti kaunti ya Kiambu, watatu hao ambao sio maafisa wa usalama, wanadaiwa kupatikana wakiwa wamevalia mavazi yanayofanana na yale ya Vikosi Vya Ulinzi KDF bila idhini.
Akizunumza na wanahabari nje ya Mahakama ya Mahakama baada ya kuondolewa kwa mashtaka hayo, Patrick Osoi alikaribisha hatua hiyo, akidai kuwa serikali iliwaita magaidi kimakosa.
Alitoa wito kwa maafisa wa usalama kuzingatia katiba wanapotekeleza majukumu yao.