Jubilee yapinga uamuzi wa kubatilisha uteuzi wa Kenta

Chama hicho kimesema kitawasilisha ombi la kupitiwa upya kwa uamuzi huo kwa mujibu wa sheria na kutumia njia zote za kisheria zinazopatikana.

Marion Bosire
1 Min Read

Chama cha Jubilee kimepinga uamuzi wa jopo la kutatua migogoro ya vyama vya kisiasa, uliobatilisha uteuzi wa Moitalel ole Kenta kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Katika taarifa ya Septemba 12, 2026, chama hicho kilisema jopo hilo liliidhinisha uteuzi wa Fred Matiang’i, Vincent Kemosi, Jeremiah Kioni, Yassir Noor, Zack Kinuthia na Dann Mwangi kuwa maafisa wa chama.

Hata hivyo, Jubilee kilisema hakikubaliani na uamuzi kuhusu Kenta, kikidai kuwa jopo hilo halikuzingatia kikamilifu hoja muhimu na ushahidi uliowasilishwa mbele yake.

Chama hicho kilisema, kwa mujibu wa rekodi zake na uthibitisho kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kabla ya mabadiliko yaliyofanywa Mei 21, 2026, Kenta alikuwa mwanachama aliyesajiliwa kihalali wa Jubilee.

Jubilee ilisema Kenta alisajiliwa kuwa mwanachama wa chama hicho mnamo Desemba 24, 2025, hivyo alitimiza sharti la uanachama alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu mnamo Januari 22, 2026.

Chama hicho kimesema kitawasilisha ombi la kupitiwa upya kwa uamuzi huo kwa mujibu wa sheria na kutumia njia zote za kisheria zinazopatikana.

Jubilee imesisitiza kujitolea kwake kwa utawala wa sheria, Katiba ya chama na misingi ya kidemokrasia inayoongoza shughuli zake, huku ikitafuta kusuluhisha mzozo huo kupitia njia za kisheria zilizowekwa.

Share This Article