CHADEMA yataka mpatanishi kutoka nje ya Tanzania

Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu alisema hawana imani na wapatanishi wa ndani.

Marion Bosire
2 Min Read

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzana CHADEMA, kimesema kwamba ili mchakato wa maridhiano ufanikiwe, wangetaka mpatanishi atoke nje ya nchi hiyo.

Kauli hii ilitolewa na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, akisema sio vizuri kutegemea watu wa ndani pekee.

Sugu ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Ikukwa, Wilaya ya Mbeya Vijijini, wakati wa ziara yake ya kutembelea Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mbeya.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Chama hicho kuruhusiwa kurejea kufanya mikutano ya hadhara baada ya takribani mwaka mmoja.

Aidha, amesema Chama chake kiko tayari kushiriki katika mazungumzo ya upatanishi yatakayoongozwa na Taasisi za Kimataifa kama Umoja wa Mataifa au Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika au Umoja wa Afrika.

Alidai kwamba kama chama, hawana imani ya kutosha na Wapatanishi wa ndani katika kutafuta suluhu ya mgawanyiko wa kisiasa uliopo nchini Tanzania kwa sasa.

Maridhiano ya kitaifa yamekuwa yakipendekezwa nchini Tanzania, kufuatia matukio ya Oktoba 29, 2025, siku ya uchaguzi mkuu na siku kadhaa baadaye.

Watu kadhaa walifariki, wengine wakajeruhiwa na mali ikaharibiwa na sasa mjadala mpana umeibuka kuhusu mustakabali wa demokrasia, haki za raia, na mwelekeo wa kisiasa wa nchi.

Share This Article