Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari na Vyuo nchini Kenya, KUPPET kimekataa nyongeza ya mishahara iliyopendekezwa na Tume ya Mishahara na Marupurupu,SRC.
Kinasema kwamba walimu hawajatendewa haki ikilinganishwa na watumishi wengine wa umma.
Katibu Mkuu wa KUPPET, Akelo Misori, alisema usawazishaji wa mishahara uliopatikana wakati wa Serikali ya Muungano Mkuu umeanza kubadilishwa, huku pengo la malipo kati ya walimu na watumishi wengine wa umma wenye viwango vinavyolingana likizidi asilimia 60.
Kulingana na chama hicho, walimu walipata nyongeza ya mishahara kupitia Makubaliano ya Pamoja ya Kazi ya kati ya shilingi 900 na shilingi 2,000, huku watumishi wengine wa umma wakinufaika na nyongeza kubwa zaidi.
KUPPET pia iliikosoa Tume ya Huduma za Walimu,TSC kwa kushindwa kulinda maslahi ya walimu, ikitaja changamoto kama mgao mdogo wa kulipia nyumba na bima ya afya ya SHA.
Walimu wengi wamelalamikia kucheleshwa kwa huduma za matibabu na hitilafu za mfumo wa SHA huku wakilazimika kulipia huduma za afya kutoka mifukoni mwao ilhali zinapaswa kugharimiwa.
Wamelalamikia pia gharama kubwa za matibabu maalum, ikiwemo vipimo vya utambuzi vinavyohusiana na matibabu ya uzazi kwa njia ya IVF.
Chama hicho kimeitaka TSC kutoa mpango mbadala wa bima ya afya iwapo SHA itaendelea kushindwa kuhudumia walimu ipasavyo.
KUPPET pia kimeonya kuwa huenda kikachagua kufuata njia ya mgomo endapo malalamiko yao hayatashughulikiwa.